Mke alikataa kuja nyumbani nikaoa mwingine

NINA mke na watoto watatu. Mke wangu alipata kazi mbali na nyumbani na anaishi huko. Ni siku nyingi hajaja nyumbani na nikimuuliza anadai hana pesa. Nimeshindwa kuvumilia na nimepata mwanamke mwingine ambaye sasa ninaishi naye na pia ana mimba yangu. Mke wangu alijua na akanipigia simu akitishia kuwa akimpata mwanamke huyo nyumbani kwetu atakiona. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nitakulaumu kwa kukimbilia kuoa mwanamke mwingine eti kwa sababu mke wako amekawia kuja nyumbani. Kabla hujachukua hatua hiyo ungejitolea mwenyewe kumtembelea huko anakofanya kazi ili ujue shida iliyopo kwani wewe ndiye mume wako. Itabidi umwambie ukweli mwanamke huyo kwamba mke wako hamtaki hapo ili aondoke kwani hujui amepanga kuchukua hatua gani.

Nashuku anidanganya

HUJAMBO shangazi? Mimi nahisi kuwa mwanamume mpenzi wangu ananidanganya. Sababu ni kuwa bado anaweka nambari ya simu ya mpenzi waliyeachana. Nashangaa ni kwa nini bado anaweka namba hiyo kama kweli waliachana. Nishauri.

Kupitia SMS

Huenda mpenzi wako aliamua kuwa wataendelea kuwa marafiki na huyo wake wa zamani hata baada ya kuachana. Kama una wasiwasi kuhusu yeye kuendelea kuwa na nambari hiyo, ni vyema ushauriane naye kuhusu jambo hilo badala ya kulinyamazia.

Nimetemwa

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 20 na nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa. Sasa amenigeuka ghafla ananiambia eti hanitaki nitafute mwingine. Nampenda sana na sijui nitafanya nini. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni muhimu ufahamu kuwa hakuna mikataba inayowekwa kudumisha uhusiano kwa hivyo mmoja wa wahusika akihisi kujiondoa kwa sababu moja au nyingine ana haki ya kufanya hivyo. Kama mwenzako amekwambia hakutaki, huna la kufanya ila kukubali uamuzi wake kwa sabu huwezi kumlazimisha akupende.

Amesema hataki kuoa
HUJAMBO shangazi? Nimekuwa na uhusiano na mwanaume fulani kwa miaka sita sasa na amekuwa akila pesa zangu tu. Sasa amenipa mimba na ananiambia hayuko tayari kuoa. Yeye anaishi Nairobi nami naishi Mombasa. Je, atanioa au la?

Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini amekuwa akila pesa zako ilhali yeye ndiye mwanaume anayefaa kukupa pesa za kugharamia mahitaji yako. Pili, sielewi ilikuwaje ukakubali kupata mimba yake bila hakikisho kutoka kwake kwamba atakuoa. Madai yake kuwa hayuko tayari ni dalili za kutaka kujitenga nawe na usishangae akikutema. Ushauri wangu ni kuwa uwe tayari kwa chochote kile kutoka kwake.

Nimembania asali

SHANGAZI nina mpenzi tunayependana sana na tumekuwa pamoja kwa mwaka mmoja sasa. Ameahidi kunioa na amekuwa akiniomba mahaba lakini naogopa kwani sijawahi kufanya hayo maishani mwangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Jambo analotaka mwenzako litategemea hiari yako wala si lazima. Hasa, tendo la ndoa linafaa kusubiri hadi watu wanapooana ingawa baadhi ya watu hukubaliana kuanza mapema. Kama unahisi huwezi kwa sasa, mwambie mwenzako na umuelezee sababu. Kama kweli anakupenda ataelewa.

Nimeambiwa anafuatafuata vidosho

MPENZI wangu alinipa mimba punde tu nilipomaliza shule ya msingi na bado tuko pamoja. Wazazi wangu wamenipeleka kusomea ualimu na sasa nimesikia fununu kuwa huyo mpenzi wangu ameshikana na wasichana wengine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Unasema umepata fununu tu kuhusu huyo mpenzi wako wala huna hakika. Tafuta jinsi ya kuthibitisha fununu hizo ili ujue ukweli. Ukipata ni ya kweli, haina haja ya kuendelea na uhusiano na mtu ambaye si mwaminifu kwako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *